ZITTO KABWE
Tuhuma za Zitto na Funzo
la Bruce Lee, Lissu na Julius Caesar
Na
Munir Abubakar, Dar es Salaam
HIVI karibuni nimemsikia
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, akiibuka na tuhuma za ajabu kwa mwanasiasa
wa aina yake kuzitoa; kwamba ametishiwa maisha akiwa Bungeni tena akituhumu
watu wa Idara muhimu katika kulinda usalama wa nchi hii.
Kauli ya Zitto si ya
kwanza kwa wanaofuatilia mambo mengi anayoyaandika kwenye mitandao mbalimbali
ya kijamii. Mara kadhaa amekuwa akiibuka na kuzusha madai kama hayo akidai kuna
watu wanapanga njama za kumuua na mara zote akiitaja Serikali.
Kama madai yake hayo
yanaukweli au ni “kiki” za kisiasa ni suala linalohitaji utafiti wa kina ambao
aghlabu makala haya kwa sasa hayawezi kufikia hitimisho, lakini kama Taifa yako
mambo lazima tuungane kuyakataa; hasa tabia hii mpya ya kila mwanasiasa kuibuka
tu na madai ya jumla jumla kuwa Serikali au vyombo vyake vinatak kumdhuru.
Niseme tu, kauli ya
Zitto, ambaye inadaiwa amelifikisha suala hilo la jinai kwa Spika wa Bunge,
badala ya Polisi, ni mwendelezo wa staili mpya hapa nchini ya wanasiasa
wanaoonekana kuishiwa hoja za kisiasa kukimbilia kudai wanatishiwa na Serikali
au vyombo vyake.
Haraka haraka niliposikia
kauli ya sasa ya Zitto na anavyoendelea kulishadidia suala hilo mitandaoni,
nikakumbuka hadithi nyingi juu ya yaliyowafika wanasiasa wengi duniani huko
nyuma katika maisha yao ya kisiasa ambapo madhara mengi waliyoyapata ilikuja
kubainika kuwa hayahusiani ni kile wengi walichoamini au kuaminishwa awali.
Nasisitiza sikatai
kuwa Zitto anaweza kutishiwa na taasisi au mtu binafsi katika Serikali, hilo ni
suala la mahusiano na ushahidi, lakini nasisitiza pia tusikatae kuwa Zitto huyo
huyo anaweza kuwa na “bifu” mbaya zaidi zinazohatarisha maisha yake na makundi
mengine ya watu wasio Serikali, lakini kisiasa, kila siku akawa anaonesha adui
yake ni Serikali tu.
Katika kuyaelewa
anayoyaleta Zitto hapa nchini hivi sasa, nimelazimika kuirejea upya fasihi
niliyopata kuisoma zamani ya mwanahistoa za masuala ya madhara ambayo viongozi
mbalimbali wa kisiasa wamekuwa wakiyapata J. Bowyer Bell, aliyeandika tasnifu “Assassin: Theory and Practice of Political
Violence. 1st Edition.”
Tasnifu
hii inatusaidia kuyaelewa madhara mbalimbali ambayo yamepata kuwakumba
wanasiasa duniani na sababu tofauti ambazo wakati fulani, baada ya uchunguzi,
ilibainika kuwa ni tofauti kabisa na sababu ambazo watu waliamini au
waliaminishwa kama Zitto anavyofanya hapa nchini.
Ni ukweli
uliodhahiri kuwa Zitto ana maadui wengi na wanajulikana. Ni vyema akaishi kwa
kujitathmini maisha yake badala ya kila mara kulaumu Serikali. Mfano, bado
usaliti wake kwa Chadema umeacha alama isiyofutika, kuna makampuni/nchi
mbalimbali ambazo amekuwa anawatumikia kisiasa na kuna wakati anabadilika na
kuibua bifu lakini kijamii, anajulikana, niseme tu kuwaumiza mabinti wengi.
Nimetaja
baadhi ya “facts” tu zinazoweza kutusaidia kuyaelewa matishio aliyonayo Zitto hasa
wakati huu pia yeye na baadhi ya wanasiasa wa upinzani wanapogongana kuweka nia
za kuwania Urais, kwa sababu bahati mbaya yeye bado anatangaza tu kuwa adui
wake ni Serikali.
Labda
tumkumbushe Bw. Zitto anachokifanya leo hapa Tanzania kimeshatoke katika kioo
halisi cha maisha ya wanasiasa na watu wengine wengi mashuhuri ambapo kile
ninachokisema kuwa mtu anaweza kuwa na maadui wengi na yeyote kati yao
akamdhuru kilisadifu. Nitatoa mifano michache.
Kama Zitto
anavyotaka kutuaminisha, akiwa amewaudhi Waislamu wa India na kila mtu akiwa
anajua adui mkubwa wa Gandhi yangekuwa makundi yenye msimamo mkali wa kiislamu,
siku ya Januari 30, 1948 alipouawa Mahatma Gandhi wa India na kijana wa dhehebu
lake la Kihindu aitwae, Nathuram
Vinayak Godse, ndipo watu walipopigwa na butwaa!
Hadithi ni
kama hiyo ya Zitto kwa mtaalamu wa filamu za Kung Fu na mwasisi wa mtindo wa mapigano wa Jeet Kune Du, Bruce Lee ambaye kila mmoja alijua maadui zake ni
wahafidhina wa Kichina waliokuwa hawataki afundishe sanaa hiyo ya Kichina kwa
Wamarekani.
Lakini
kumbe, tofauti na adui huyo ambaye hata Bruce Lee alikuwa akimtangaza
hadharani, adui halisi aliyekuja kuhitimisha maisha yake akabainika ni afya
yake, tabia yake ya kutopumzika na mazoezi ya nguvu. Ndio maana mabingwa wote
wa tiba wakathibitisdha kuwa Julai 20, 1973 alipofariki usingizini, kilikuwa
kifo kilichotokana na madhara hayo katika ubongo na dawa alizokunwa.
Lakini
yapo pia mafunzo kuhusu mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israeli Yitzhaki
Rabin ambaye maadui wanaoisaka roho yake wangeweza kuwa Wapalestina waliokuwa
wanaona wanaonewa lakini na wanasiasa wenzake wa chama cha upinzani cha Likud.
Lakini
siku anauawa Novemba 4, 1995 na kijana wa Kiyahudi, Yigal Amir, ndipo dunia
ikajua tu kwamba kumbe mitazamo tofauti ya kisiasa na siasa za ushindani
zinaweza kumtengenezea mwanasiasa maadui miongoni mwa vijana na watu wa
kawaida.
Tunajifunza
pia kutoka kifo cha mtawala wa zamani wa Roma Julius Caesar, ambaye baada ya
kujikinga kwa muda mrefu na husda za maadui zake wa nje ya Dola ya Rumi
aliyokuwa ameijenga kwa mabavu, ni washirika wake wa ndani kisiasa (maseneta
akiwemo kijana wake Brutus) waliosshiriki kumuua kwa kumchoma visu 23 akiwa
kwenye jumba la Maonesho la Pompey (Pompey Theatre mnamo mwaka 44BC).
Hoja yangu hapa ni kwamba
Zitto aache kuudanganya umma kwanza kwa kila mara kuonesha kuwa ana adui mmoja
tu; Serikali ili siku maadui wengine wakimdhuru au akinusurika na madhara hayo Serikali
ichafuke. Hii ni kiki ya kijinga sana ya kisiasa.
Wakati mpaka leo wengi
bado wanatafakari ni nani hasa amehusika kumdhuru Tundu Lissu, ninachokiona, na
ambacho naamini hata wachunguzi wa suala la Lissu inawachukua muda ni tabia hii
hii ya wanasiasa wetu nchini kuficha madhambi au maadui zao wengine na kuuandaa
umma kujua adui wao ni mmoja tu; Serikali.
Kama Zitto anavyotamani
umma umwanini, tumeona katika sakata la Tundu Lissu naye wakati huo na hata
sasa amejaribu sana kuuhadaa umma ionekane kama vile Serikali ndiyo adui wake pekee
ili linapomtokea lolote, Serikali ichafuke.
Kama ambavyo leo
tunamuona Zitto anaanza kwa mara kadhaa kurudia rudia kuwa eti kuna maafisa wa
Serikali wanapanga mkudhuru, Lissu naye alianza kwa lawama hizo hizo, mara
akitoa namba za gari aliyodai inamfuatilia na kudai ni la Serikali mara kaamka
tu kitandani Nairobi hata akiwa hajui tarehe ya siku hiyo akaanza kuropoka ni
Serikali.
Nafahamu, kwa kuwa wote
nimebahatika kuwa karibu na familia zote, wote, Zitto na Lissu, wanamatishio
mengi kwa maadui zake kadhaa na najua wataalamu wa Serikali wenye uwezo wa
kuona zaidi ya tunayoyaona, wameshapata kuwaonya wachukue hatua au wapewe msaada
ulinzi, wamekuwa wakikataa.
Ni kwa sadfa au bahati mbaya
tena, wanasiasa hawa wawili, pamoja na kukataa ushauri au ofa ya kupatiwa
msaada wa ulinzi, kwa mujibu wa duru za familia zao, na huku wakijua hatari
walizonazo kutokana na njama za maadui zao, wamekuwa na kiburi cha kisiasa cha
kuendelea kuitusi na kuituhumu Serikali.
Mtu angeweza kujiuliza
kwa nini Zitto bado anaona kuna faida kuilaumu Serikali wakati anajua matisho
ya sababu nyingine aliyonayo? Jibu la utafiti wangu ni kwamba wanaomjua kisiasa
Zitto Kabwe watakubaliana nami kuwa ni kweli sio yule wa zama za Buzwagi.
Amechuja sana na kama
kuna jambo amebaki nalo kwa sasa baada ya zile zama za kuibua ufisadi mkubwa
mkubwa na kwa ushahidi mzito kwisha, basi ni kuokoteza okoteza hoja walau
aonekane bado yupo katika siasa. Hivyo anahaha kusaka kiki za kisiasa.
Yule Zitto Kabwe wa
Daruso na Zitto Kabwe wa Buzwagi, mwanasiasa kijana aliyekuwa upande wa
wanyonge na upande wa maendeleo sio wa sasa. Mazingira na hali halisi
vimemfanya kwa sasa alazimike kuwa upande wa mabeberu akiwaunga mkono katika
mambo mbalimbali. Hivyo maisha yake nchini yamebaki ya kuungaunga kisiasa.
Kuitaja Serikali kuwa inataka kukudhuru yeye anaona kunalipa!
Nimesema hapo awali kuwa
kuna kauli anazitoa kwa sasa Zitto zinafikirisha na ni vyema sisi Watanzania
tukazitafakari kwa kina. Zitto anatamani kutembelea katika nadharia ya Lissu;
kwamba kwanza aanze kuonesha huruma kuwa kuna watu wanataka kumdhuru, ili siku likimtokea
kweli, iwe kwa sababu yoyote, ilaumiwe Serikali na kila mtu awe upande wake.
Kama alivyoanza Lissu,
sasa hivi unamuona Zitto naye mara kwa mara anatamka kuwa “amesikia” mara
“ameelezwa” kuwa kuna mipango ya maafisa wa Serikali kumdhuru. Hadithi hizi zinapita
mule mule kwenye mikono ya Lissu, kwenye dhana ya Bruce Lee na kwenye akili na
maisha ya wafuasi wa Gandhi na wale wa Rabin.
Hapa nisipoteze,
ninachokiona hakuna cha Usalama wa Taifa wala nini, Zitto anakoleza stori
kuhalalisha kiki yake ya kisiasa ili ikitokea akajidhuru, kudhuriwa na maadui
zake wengine au lolote likamtokea moja kwa moja ailaumu Serikali kama njia ya
kupanda chati tena.
Nionavyo, kwa sasa
hatupaswi kuendelea kulea usanii wa aina hii, niwaombe tu Watanzania tukatae
majaribio yoyote yenye lengo la kisiasa kuipaka matope nchi yetu, tukatae
wanasiasa hawa ambao wako tayari kudhurika au kutunga kudhurika au kuficha
madhambi waliyonayo ambayo yanaweza kuwa chanzo cha kudhurika kwao ilimradi tu ikitokea
waichafue nchi yetu. Tukatae. Tusikubali.
|
No comments:
Post a Comment